Nape Ahoji Kuhusu Uhalali wa Harambee za CHADEMA
CHAMA Cha Mapinduzi kimeukosoa utaratibu wa Chadema wa kufanya harambee ili kukusanya fedha za kuendeshea chama hicho, kikiuita kuwa ni usanii unaolenga kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yanayodaiwa kutolewa na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Aliyeibua tuhuma hizi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi ya chama hicho, Nape Nnauye ambaye anasema Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie huku viongozi wake wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. “Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanya kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni." anasema Nape.
Nape amesisitiza kuwa CCM wanao ushahidi kuhusu zinakotoka fedha na mikataba wanayoingia Chadema na wafadhili hao na kudai kuwa kama hawatasema wenyewe basi yeye (Nape) ipo siku atawasaidia kwa kutaja wafadhili hao na kuanika hadarani mikataba hiyo. "Kwanini mabilioni hayo yanatolewa kwa Chadema wakati huu ambapo sasa Tanzania imo katika kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? Na Je ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe? " Nape anahoji.
Anaongeza kuwa, hatua hiyo ya Chadema itaitumbukiza Tanzania katika machafuko yasiyoisha, kama ambavyo inashuhudiwa katika baadhi ya nchi zenye rasilimali kama madini ambako nchi zenye utajiri wa fedha zilijipenyeza kupitia walioitwa wapambanaji wa uhuru na haki katika nchi hizo na hadi sasa hakuna amani.
Hata hivyo Chadema kupitia msemaji wake John Mnyika, kimejibu madai hayo akisema CCM inaumizwa na jinsi watu wanavyojitokeza kukiunga mkono chama hicho. “Ni ukweli ulio wazi kwamba Chadema imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli,” anasema Mnyika na kuongeza,
“Madai ya CCM kuwa tumepokea au tutapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kumtaka Nape ataje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje tumepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.”
SOURCE: MCL
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII