Polisi Aliyefyatua Bomu na Kusababisha Kifo Cha Mwangosi Akamatwa



POLISI alifyatua bomu kwa karibu na kusababisha kifo cha Mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote, Fikra Pevu limefahamishwa.

Taarifa za kutoka Iringa zimeeleza kwamba kushitakiwa kwa askari huyo, kunafuatia kukamilika kwa uchunguzi wa awali ambao unathibitisha pasi shaka kwamba bomu alilofyatua ndilo lililosababisha kifo cha mwandishi huyo wa habari.

Imethibitishwa kwamba kilichousambaza mwili wa mwandishi huyo ni bomu maalumu linalorushwa kwa kutumia bunduki kwa nia ya kusambaza watu waliokusanyika kwa nia ya kutenda uhalifu na lilirushwa kwa karibu mno kinyume cha masharti na kanuni za matumizi yake.

Bomu hilo hutakiwa kurushwa kutoka umbali wa mita kati ya60 na 80, wakati askari huyo alilirusha kwa karibu mno na akimlenga mwandishi Mwangosi.

Katika tukio hilo, bomu hilo liliusambaratisha mwili wa Mwangosi na kumjeruhi ofisa mmoja wa polisi ambaye anaelezwa kutaka kumsaidia mwandishi huyo ambaye alikua akipigwa na polisi wenzake.

Marehemu Mwangosi aliuawa Jumapili iliyopita katika kijijini cha Nyololo, wilayani Mufindi, mkoani Iringa katika tukio ambalo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikuwa wakifungua tawi la chama chao, huku Polisi wakitumia nguvu kubwa kuzuia uzinduzi wa tawi hilo.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs