Pinda aeleza alivyozomewa Mwanza

BongoNewz
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuzomewa kwenye mkutano wa hadhara jijini Mwanza kisha msafara wake kupopolewa mawe, kiongozi huyo amesema kitendo hicho kimemtisha na kusema upo uwezekano mkubwa wa viongozi wengine wa kitaifa kuanza kukumbana na hali hiyo. Alisema hii ni mara yake ya kwanza kukumbana na zomeazomea, hivyo lazima kero zinazowasibu wananchi zitatuliwe kwani hali hiyo siyo nzuri kutokea kwa kiongozi wa taifa kama yeye.

Pinda aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku saba mkoani Mwanza, kilichofanyika kwenye ukumbi wa jiji la Mwanza. “Kwa kweli hali ya jana (juzi), ilinitisha sana. Kama mimi nimezomewa, kiongozi gani atakayesalimika kuzomewa akienda uwanjani hapo? “Wakati hali hiyo ikitokea, mbunge wa Jimbo la Nyamagana, jijini Mwanza, Ezekiel Wenje, aliniambia sababu hiyo ni kutokana na vijana kuchukizwa na mienendo ya baadhi ya viongozi wa CCM. “Na akaniambia Wenje kwamba tangu umalizike uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, CCM haijafanya mkutano eneo hilo kuzungumzia kero za wananchi… sasa hii ni hatari sana,” alisema Pinda huku akionekana kusononeshwa na hali hiyo.

Juzi, Pinda alishindwa kuendelea kuhutubia mkutano wake wa hadhara kwa muda, katika viwanja vya Sahara jijini Mwanza baada ya kuzomewa wakati akitaka kuhutubia. Mbali ya kuzomewa kwa kiongozi huyo, maarufu kwa jina la ‘Mtoto wa Mkulima’, baadhi ya magari yaliyokuwa kwenye msafara wake yalipondwa mawe kwenye uwanja huo wa Sahara wakati msafara wake ukiondoka, jambo lililosababisha taharuki kubwa.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kitaifa kama Pinda kuzomewa hadharani mkoani Mwanza na hali hiyo ilionekana pia kumtisha mkuu wa mkoa huo, Evarist Welle Ndikilo, na kamati yote ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Kuhusu Meli za mafuta za Irani Kupeperusha bendera ya Tanzania
Akijibu swali la mwandishi wa habari hizi, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na serikali kuhusiana na tuhuma ya meli za Iran kutumia bendera ya Tanzania kusafirisha mafuta baharini kinyume na sheria, Pinda alikiri kuwepo kwa hali hiyo. Alisema utata huo umeilazimisha serikali kuzifutia usajili meli hizo zilizosajiliwa visiwani Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kumchukulia hatua ya kumsimamisha kazi aliyekuwa wakala wa meli wa Zanzibar, huko Dubai. “Ni kweli hili tatizo lilijitokeza kwa meli za Iran kutumia bendera yetu. Lakini tulifanya uchunguzi na tukabaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kupitia kwa wakala wa meli wa Zanzibar aliyeko huko Dubai. “Baada ya kubaini haya, serikali iliamua kumsimamisha kazi wakala huyo na baadaye kuzifutia usajili meli za Iran,” alibainisha Waziri Pinda wakati akijibu swali hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs