SAINTFIET ADAI TFF IMEIPENDELEA SIMBA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Tom Saintfiet, ameiponda ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo kwa mujibu wake, imewapendelea wapinzani wao, Simba. Ratiba hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati ligi ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15, mwaka huu.
Akizungumza na Gazeti la Championi Jumatatu, Saintfiet alisema ratiba hiyo imewapendelea Simba kwa kuwa timu hiyo itacheza mechi nne mfululizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, itakaoutumia kama uwanja wa nyumbani. Saintfiet alisema ratiba hiyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa, kwa lengo la kuweka utaratibu kuwa, timu ikicheza mechi moja nyumbani, inayofuata iwe ugenini. “Ujue nashindwa kuielewa hii ratiba ambayo inaonekana kuibeba Simba, inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa kabla ya kuanza kwa ligi.
“Haiwezekani timu moja icheze mechi nne mfululizo katika uwanja wa nyumbani, mbona inajulikana timu ikicheza mechi ya kwanza nyumbani mchezo unaofuata lazima iende ugenini! “Lakini wenzetu wenyewe mechi nne mfululizo watacheza nyumbani, Uwanja wa Taifa. Watashindwa kufahamu miundombinu ya viwanja vingine,” alisema Saintfiet.
Mechi hizo nne ambazo Simba itacheza nyimbani ni dhidi ya African Lyon, JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons. Michezo yote hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa.
SOURCE: GPL
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII