UAMSHO WACHOMA OFISI YA CCM UNGUJA

MASKANI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Kashorora iliyopo Rahaleo, mjini Unguja, imelipuliwa kwa moto juzi jioni na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa kikundi cha Uamsho.

Aidha, moto huo umesababisha hasara kubwa ya mali, ikiwa ni pamoja na samani zilizokuwa zinauzwa katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Aziz Juma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa viongozi wa maskani hiyo na kusema uchunguzi wa awali unaonesha kikundi cha Uamsho kuhusika na tukio hilo.

Alisema watu hao wanaodhaniwa ni wafuasi wa Uamsho walikuwa wakitoka maeneo ya Daraja Bovu na Msikiti wa Shurba, baada ya kumaliza mihadhara ya dini.

“Uchunguzi wetu wa awali wa tukio hili unaonesha wazi wazi kuhusika kwa kikundi cha Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema linafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha vikundi vya dini kuchukua hatua ya kushambulia majengo na maskani za CCM.

Alisema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kuhusika na tukio hilo ambapo alikamatwa mara baada ya Jeshi la Polisi kufika katika eneo la tukio na kuanza kuwatawanya watu waliovamia maskani hiyo.

Kiongozi mwandamizi wa maskani hiyo, Rajab Bakari alisema tukio hilo lilitokea katika majira ya saa 12 jioni baada ya kundi la vijana takribani 300 waliokuwa wakiandamana huku wakiwa na bendera za Uamsho kufika eneo hilo wakitokea mitaa ya Magomeni na Daraja Bovu.

Walipofika katika maskani ya Kashorora walianza kurusha mawe na kuyaondoa mabango ya matangazo pamoja na ubao wake ulioandikwa maneno yaliyokuwa yakisisitiza ‘kudumu kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’.

“Walianza kurusha mawe na sisi tukaingia ndani ya maskani yetu na hapo walivamia na kuanza kuwasha moto ulioharibu vibaya mali za wafanyabiashara waliokuwa wakiuza samani, yakiwamo makochi,” alisema Bakari.

Aliongeza kuwa kwa muda mrefu baadhi ya vikundi na watu wamekuwa wakichukizwa na maneno katika ubao wa matangazo wa maskani hiyo ambayo imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Muungano, huko baadhi ya maneno yakisema wasiotaka Muungano warudi makwao.

Mmoja wa wafanyabiashara waliopoteza mali zao ni Khalid Manzi, ambaye anasema amepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 10. “Nimepata hasara kubwa ya mali yangu, makochi ambayo huyachukua kutoka Tanzania Bara na kuyaleta Unguja kwa ajili ya biashara,” alisema Manzi.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi amelaani vitendo vinavyofanywa na watu wanaojichukulia sheria mikononi mwao na kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema kuna watu ambao kwa sasa wanaonekana kuchoshwa na amani na utulivu uliopo Zanzibar, hivyo kuibua chokochoko za kutaka vurugu na uhasama wa kisiasa.

“Nimesikitishwa sana na vitendo hivyo vilivyofanywa na kundi la watu ambavyo vinaashiria moja kwa moja uvunjifu wa amani na kutaka kuwarudisha watu kule walikotoka ikiwemo siasa za fujo na uhasama,” alisema Mwinyi.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya Kamati Maalumu ya CCM- Zanzibar, Issa Haji Ussi alisema CCM inalaani tukio hilo la uharibifu wa maskani ya Kachorora na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Uamsho na kusema hicho sio kikundi cha dini tu, lakini upo uhusiano wa vyama vya kisiasa.

“CCM imesikitishwa sana na tukio hilo ambalo lengo lake ni kurudisha nyuma juhudi za vyama vya siasa kufanya kazi zake za kuhamasisha wafuasi wake wakiwemo wanachama...sisi tunachojua hiki si kikundi cha dini pekee yake, lakini kuna mkono wa vyama vya siasa,” alisema.

Hata hivyo, Ussi hakukitaja chama cha siasa kinachotuhumiwa kujishughulisha na vitendo hivyo ambavyo kwa kawaida vinaonekana kufanywa kwa kutumia mgongo wa jumuiya ya Uamsho, na kutoa onyo kwa kikundi hicho.

Maskani ya Kashorora ni miongoni mwa maskani kubwa za CCM ikiwa na jengo la ghorofa moja.

Kuibuka kwa matukio hayo ya vurugu za Uamsho kumekuja miezi kadhaa tangu kilipohusishwa na uchomaji wa makanisa na baa, matukio yaliyolaaniwa na wafuasi wa dini zote, viongozi wa kisiasa na serikali, huku likiwekwa angalizo la kukichunguza kikundi hicho hatari kwa amani na usalama wa nchi.

SOURCE: JF 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs