Wanaotaka kumng’oa Mufti wakamatwa

JESHI la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutaka kumuondoa madarakani Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Shaaban Simba na viongozi wenzake.

Watu hao ambao hawakutajwa majina yao, wanashikiliwa kwa mahojiano, huku watu wengine wanane ambao wanatuhumiwa kuhusika na tuhuma hizo, wakitakiwa kujisalimisha wenyewe kabla jeshi hilo halijachukua hatua za kisheria dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Jeshi la Polisi limechukua hatua hiyo kwa kuwa ni kosa kisheria kutaka kumng’oa mtu madarakani bila kufuata utaratibu.

“Tayari tumepokea malalamiko na kufungua jalada la kesi kuhusu tuhuma hizo ambazo lengo lake ni kutumia nguvu na mabavu, kwani hali hiyo iliashiria uvunjifu wa amani.

“Ni jukumu la Serikali kupitia vyombo vya dola, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, kuhakikisha taasisi zote ni salama, ikiwamo hiyo BAKWATA kwa sababu imesajiliwa kisheria.

“Ni wajibu wetu kuwalinda viongozi walioko madarakani mpaka pale taratibu za kiutawala au kikatiba zitakapowaondoa madarakani na ndiyo maana hawa tumewakamata kwa kosa la kutaka kumwondoa madarakani Mufti,” alisema Kamanda Kova.

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, baada ya malalamiko hayo na kufungua jalada hilo, watu mbalimbali wameanza kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo na wakigundulika kuhusika Serikali itachukua hatua za kisheria dhidi yao.

“Lazima ifahamike wazi kuwa, Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua madhubuti za kisheria pale ambapo kundi lolote la kidini ama la kisiasa litakapobainika kuhatarisha usalama wa wananchi wasio na hatia.

“Tunawahakikishia uongozi wa BAKWATA, kwamba Jeshi la Polisi lipo makini, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wale wote wanaotaka kuvunja amani.

“Katika hili tutakabiliana kikamilifu na kundi dogo au kubwa litakalojaribu kuvamia Ofisi za BAKWATA, NECTA au Mamlaka nyingine yoyote, nasema tuko imara,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kova amewataka wananchi na wafuasi wa vikundi visivyo rasmi wasijiingize katika mambo yasiyofaa, kwani watakaofanya uovu wowote watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs