Waziri wa JK ahenyeshwa na Mratibu wa Kata

BongoNewz
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI-Elimu), Kassim Majaliwa, ameonja machungu ya uongozi, baada ya kutunishiwa msuli na Mratibu wa Elimu wa Kata ya Mvumi Mission, Charles Ulanga, kutokana na kuzuiwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo. Lakini pamoja na Waziri Majaliwa kutoa kauli hiyo, Mratibu huyo amesema atagombea nafasi hiyo, kwa sababu ni haki yake ya kikatiba.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na uamuzi wake, Waziri Majaliwa alisema kitendo cha mratibu kugombea nafasi hiyo ni kukiuka sheria. Licha ya kauli hiyo, mratibu huyo amechukua fomu kwa mara nyingine kwa ajili ya kutetea nafasi yake hiyo ya uenyekiti.

Waziri Majaliwa, alisema nafasi ya Uratibu Elimu Kata, ni kazi ya kila siku ambayo haipaswi kuambatana na shughuli za kisiasa.

“Kitendo cha Mratibu Elimu Kata kugombea nafasi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kwenda kinyume na kanuni za utumishi.

“Haiwezekani akaweza kutenda haki kwa watu anaowaongoza na wala hatotenda haki kwa mwajiri wake, kwa kuwa katika harakati za kisiasa ni lazima ataacha nafasi moja na kutumikia zaidi nafasi nyingine,” alisema Majaliwa. Alisema Mkurugenzi wa Halmashauri, ana wajibu wa kutoa majibu ya mratibu kuhusu mratibu huyo kutumikia nafasi katika chama, wakati ni muajiriwa wa halmashauri.

Malalamiko ya kugombea kwa Ulanga katika nafasi hiyo, yalikuja baada ya baadhi ya walimu anaowaongoza kuandika barua kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino, kupinga jina lake, kupitishwa kwa madai kuwa kiongozi wao huyo hawatendei haki. Pamoja na mambo mengine, barua hiyo ilimtaka mratibu huyo kuchagua nafasi moja, kwani kutaka nafasi zote zinapunguza ufanisi wake wa kazi.

Kwa upande wake mgombea huyo, alisema anayo haki ya kugombea na ana haki pia ya kuchaguliwa kwa ajili ya kuwaongoza, huku akitolea mfano wa Rais kwamba licha ya majukumu mengi, lakini bado ni mwenyekiti wa CCM.

“Haya ni majungu tu yanayotengenezwa dhidi yangu na mimi nitaendelea kugombea na wanachama ndio wenye haki ya kumchagua mtu au kutokumchagua, lakini suala la kazi haliwezi kunizuia kuendelea na harakati zangu za kisiasa,” alisema.

SOURCE: JF
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs