Pichani Juu na Chini ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo ambapo amezungumzia suala la mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Nchi ya Tanzania na Malawi.Kulia ni  Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa John Haule Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria cha Wizara hiyo Bi.Irene Kasanja.
Pichani ni waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini waliohudhuria mkutano wa Waziri Membe.

Serikali ya Tanzania imeijia juu Malawi kuhusiana na suala la mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa na kueleza kuwa ina  uwezo wa kulipeleka kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe amesema serikali inaweza kwenda ICJ na kushinda kesi na ziwa Nyasa kuendelea kubaki na ramani yake ya awali ya enzi na enzi.

Hata hivyo, hadi sasa serikali ya Malawi imesusia vikao viwili ambavyo vilipangwa kufanyika kwa lengo la kutatua na kupata jawabu ya mgogoro huo ambao umekuna vichwa vya viongozi wa nchi hizo mbili. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mh.  Bernard Membe amesema hatuwezi kukubali mtu mmoja asije na taratibu zisifuatwe, na kufafanua kuwa tatizo hilo litakiwisha kipindi cha Rais Jakaya Kikwete na kuwa litamalizika kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015.

Katika maelezo yake Mh. Membe amesema hadi sasa Serikali  ya Tanzania haijatangaza rasmi kujiunga na ICJ, ingawa Malawi tayari ni Mwanachama, hivyo endapo nchi ikitangaza kujiunga hata sasa inaweza kukimbilia ICJ na kuibuka kidedea. Ingawa Mh. Membe alishindwa kueleza sababu ya Tanzania kutojiunga hadi sasa,  amefafanua kuwa uwezo wa kushinda ni mkubwa kutokana na baadhi ya migogoro ya aina hiyo kutatuliwa bila ubaguzi kwani Mahakama hiyo itachora ramani ile ile ambayo ipo tangu zamani.

Alienda mbali zaidi na kueleza kuwa, Serikali ya Tanzania haijafikiria kukimbilia ICJ kwa kuamini kuwa suala hilo linaweza kutatulika kwa njia ya amani. Kwa mujibu wa kauli yake, kama mazungumzo hayo yatakwama  Serikali itaweza kulipeleka suala hilo kwenye Umoja wa Afrika kwa ajili ya kutatuliwa kwa amani zaidi.

Hivyo, Serikali haipendi kuona mgogoro huo ukiendeshwa kishabiki hasa kwa Serikali ya Malawi kutokana na kukaidi baadhi ya makubaliano waliyofikiwa awali. Ametumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi kwamba, kama mazungumzo baina yao yatakwama  Serikali inaweza kulipeleka suala hilo kwa wazee wenye busara Marais wastaafu wa Afrika. Aidha Mh. Membe ametumia nafasi hiyo kuwatoa wasiwasi raia wa Tanzania wanaoishi karibu na eneo hilo kuwa hakuna vita yeyote itakayoweza kutokea hivyo waendelee na shughuli zao za kila siku za uzalishaji kama kawaida.