MTIKILA AIBUA MAPYA KATIKA MCHAKATO WA KATIBA

 
MAKUNDI maalumu jana yaliendelea kutoa maoni yao kwenye mchakato wa Katiba Mpya, huku DP kikipendekeza Rais aapishwe baada ya siku 90 tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Mbali na maoni hayo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji Christopher Mtikila, makundi mengine; wakulima, wafugaji, wanahabari na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) nayo yalijitokeza kutoa moyoni.
Mtikila alisema kipindi hicho cha siku 90 kitatoa fursa kwa watu wanaotaka kuwasilisha pingamizi dhidi ya ushindi wa Rais mteule kufanya hivyo, kabla ya kuapishwa.
Alisema pingamizi linaweza kufanyiwa kazi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu ili kuhakikisha kuwa taifa linapata kiongozi halali mwenye ridhaa ya wananchi.
“Pia tunataka kinga ya Rais ikome pale anapomaliza muda wake wa uongozi, kama alifanya makosa yoyote ya jinai aweze kushtakiwa ili kujenga nidhamu ya uongozi katika ofisi ya umma. Utaratibu wa kumwondoa madarakani uimarishwe asisubiriwe hadi amalize muda wake wa uongozi.” Alisema kuwa Katiba ya nchi inapaswa kuwa mali ya wananchi wenyewe ili watawala wasijihusishe katika kuwaundia wananchi Katiba kama ilivyo kwa mchakato unaoendelea sasa wa kupata Katiba Mpya.
“Kumekuwa na hoja ya kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika, hilo ni jambo muhimu na watu kutoka Tanganyika ni lazima wawe na Serikali yao ndani ya mipaka ya ardhi yao kupitia Katiba Mpya,” alisisitiza Mchungaji Mtikila.
Aliongeza kuwa nafasi za wabunge wa viti maalumu bungeni ziondolewe ili viti hivyo vishindaniwe kidemokrasia. Alisema wanawake wanatakiwa waelimishwe na kupikwa ili wahimili ushindani katika medani za kisiasa. Alisema kuwa taifa linahitaji viongozi bora na siyo kustarehesha jinsia.

Jukwaa la Wahariri
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limependekeza Katiba ijayo kutambua uhuru wa vyombo vya habari, haki ya kupata habari na uhuru wa kutoa mawazo. “Kwa Katiba hii na sheria nyingine yoyote isiyoendana na Katiba hii, milele haitaruhusiwa kudhibiti habari nchini Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.TEF ilisema kuwa haitakiwi kuwe na vikwazo katika kuanzisha magazeti  au vyombo vya habari binafsi, kwamba wahariri na wachapishaji wa magazeti na vyombo vingine vya habari hawatakiwi kudhibitiwa au kuingiliwa na Serikali.
“Chombo chochote cha habari chenye wajibu wa kusambaza taarifa kwa jamii ambacho kinachapisha taarifa kuhusu, au dhidi ya mtu yeyote kinawajibika kutoa fursa ya kuchapisha mawazo ya upande wa pili, ikiwa yapo, kutoka kwa mtu ambaye taarifa au chapisho linamhusu,” ilieleza taarifa hiyo.
Vilevile, wamependekeza kuwe na sheria ya Bunge ya kuanzisha Baraza la Habari la Taifa, ndani ya miezi sita tangu siku ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya, baraza ambalo litakuwa na wajumbe 15 kutoka katika taaluma mbalimbali.
“Wajibu wa Baraza la Habari la Taifa itakuwa ni kusimamia vyombo vya habari, kuweka viwango vya kitaaluma kwa vyombo vya habari, kufuatilia utekelezaji wa viwango vilivyowekwa, kukuza taaluma na weledi katika vyombo vya habari,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza;
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs