KIZAAZAA: MWANAFUNZI CBE ALIYEFARIKI AONEKANA AKIWA HAI


Stori: Chande Abdallah na Denis Mtima, MWANZA
KWELI dunia ina mambo! Kijana Abel Dafe 21, (pichani) mkazi wa Kayenze, Mwaloni jijini Mwanza amezua sintofahamu ya aina yake baada ya kudaiwa kufariki dunia na maiti yake kuzikwa wiki chache zilizopita na baadaye kuonekana akiwa hai, bali denti wa Chuo cha Biashara (CBE) Tawi la Mwanza ndiye akidaiwa kufa.
Desemba 2, mwaka huu, Abel alidaiwa kufa maji akiogelea katika Ziwa Victoria na mwili wake kuthibitishwa na mjomba’ake, mwili ukapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kabla ya kusafirishwa Sengerema kwa maziko Desemba 4.
Akizungumza na waandishi wetu juzi, mtu wa karibu wa Abel aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel alisema baada ya kumaliza mazishi, familia ilirudi Kayenze, Lakini yeye Desemba 17  mwaka huu ghafla alionana na Abel akiwa mzima wa afya maeneo ya Mwaloni.
Alisema alimuweka chini ya ulinzi na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Kayenze na kutoa taarifa kwa ndugu waliokuwa Sengerema ambao walifika na kujionea marehemu akiwa hai!
Kituoni hapo, Abel alikataa katakata kuwa yeye hakufa alikuwa kwenye misele yake ila alipoteza simu ndiyo maana hakuwa na mawasiliano na nduguze.
Ndugu hawakuyaamini mwaelezo hayo, wakati mwingine walitaka asiwakaribie maana ni mzimu, lakini wakiwa katika maswali mengi juu ya Abel yupi aliyezikwa, walipata taarifa kituoni hapo kuwa maiti waliyemzika Sengerema anaitwa Manyama Chimwejo na nduguze  wamepatikana.
Polisi wakaitaka familia hiyo ya Abel kukaa na familia ya Manyama kujadili hatima, kama watafukua maiti hiyo na kwenda kumzika upya Kigoma au watamwacha hukohuko Sengerema alipozikwa awali.
Akizungumza kwa simanzi, Abel (aliyedhaniwa kufa) alisema ndugu zake wanachojua waliyemzika ndiye Abel bali amefufuka.
“Ndugu zangu hawaamini kama mimi ni mzima hivyo napata tabu sana kwa kuwa kila mtu ananipigia simu kuniuliza. Mimi sikufa, nilikuwa nyumbani kwangu, tatizo lilikuwa ni mawasiliano, nilipoteza simu,” alisema Abel.
Kwa upande wa pili, kaka wa marehemu aliyejitokeza kudai maiti ya mdogo wake aliyezikwa kimakosa aliyejitambulisha kwa jina la Christopher Chimwejo alimtaja Manyama Chimwejo (20) kuwa kweli alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la Mwanza mwaka wa kwanza na alifika kuishi naye mapema mwezi huu baada ya chuo kufungwa.
Alisema Manyama alitoweka nyumbani kwake ghafla maeneo ya Mwaloni na baada ya hapo hakumuona tena jambo lililomfanya atoe taarifa polisi.
Hata hivyo, sakata hilo lilimalizika Desemba 21, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Kirumba D ambapo pande zote mbili zilikutana na kukubaliana kuacha kaburi la marehemu Manyama liendelee kuwa Sengerema licha ya kwamba familia hiyo haiamini kama mwanafunzi huyo alifariki dunia.
“Hapa kuna kitu, sisi hatujafiwa na ndugu yetu, tumechezewa. Kama ndugu yenu aliyekufa amerudi hata ndugu yetu pia atarudi tu, ngojeni kwanza tukatambike kwetu Kigoma,” alisema kaka huyo wa marehemu.
SOURCE : GPL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs