CCM yalaani shambulio la tindikali dhidi ya Sheikh Fadhili Soraga
Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha kinyama
alichofanyiwa Sheikh Fadhili Soraga cha kumwagiwa tindikali sehemu ya
uso na kifuani. Sheikh Soraga ni mtu maarufu hapa Zanzibar kwani huwa
anashiriki katika shughuli mbali mbali za kidini hapa nchini, yeye ni
Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar. Sheikh Soraga amefanyiwa unyama huo na
watu wasiojuulikana wakati akitoka kwenye mazowezi ya viungoasubuhi ya
leo.
Sheikh Soraga ni miongoni mwa masheikh wachache hapa zanzibar wenye
kuheshimika na kueleweka. Hivi karibuni Sheikh Soraga alitoa hutuba
nzuri na fasaha kwenye sala ya Eid-Haji juu ya kuimarisha amani na
utulivu katika visiwa vyetu vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Khutba
hiyo aliitoa mbele ya viongozi wakubwa wakitaifa waliohudhuria katika
sala hio, miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa
kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharifu Hamadi, Rais Mstaau wa
awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume .a viongozi wengine
kadhaa.
Siku hiyo hiyo katika Baraza la Iddi lililofanyika katika Ukumbi wa
Salama Bwawani Sheikh Soraga wakati akitoa khutba ya utangulizi aliwaasa
tena wazanzibari na watanzania kwa ujumla juu ya umuhimu wa amani,
lakini katika hafla hiyo Sheikh Soraga alikwenda mbali zaidi kwani
alitoa takwimu za hasara iliyoipata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Jamhuri ya Muungano, mashirikaya watu binafsi na ya Umma, taasisi za
Kidini pamoja na vyama vya Siasa hasa Chama Cha Mapinduzi kufuatia
vurugu mbali mbali zilizokuwa zikifanywa na Uamsho.
Vitendo vya kumwagiwa watu tindikali hapa Zanzubar vimeanza siku
nyingi. Kama tutakumbuka mnamo mwaka 1995 Kada wa Chama Cha Mapinduzi
ndugu Ali Mwinyi Msuko alimwagiwa tindikali na watu wasiojuulikana huko
Wete Pemba, mwaka 2007 wakati zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapigakura huko Pemba Sheha mmoja alimwagiwa tindi kali, na mwaka
uliopita Ndu. Rashid Ali Juma Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Zanzibar
nae alimwagiwa tindikali na watu wasiojuulikana na leo hii Sheikh
Fadhil Soraga Katibu wa Mufti Muu wa Zanzibar nae amemwagiwa tindikali
pia na watu wasiojuulikana.
Chama Cha Mapinduzi kinasema kimechoka kusikia vitendo hivi vya
kinyama vya kumwagiwa watu tindikali na watu wasiokuulikana. Tunaviomba
vyombo vya Dola kuwatafuta watu hawa waovu wasio na huruma na wenzao ili
wakamatwe waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria, na kama Jeshi
letu la Polisi uwezo wake ni mdogo wa kuuwafichua wahalifu hawa basi ni
vyema wakaomba msaada kwenye vyombo vya upelelezi vya Kimataifa kama
vile INTAPOL.
Mwisho Chama Cha Mapinduzi kinawaomba wananchi wote wapenda amani na
utulivu kumuombea duwa Mwalimu wetu Sheikh Fadhil Soraga Mwenyezi Mungu
ampe moyo wa subira yeye na familia yake na amjaalie wepesi ili apone
haraka. Sheikh Soraga hivi sasa amesafirishwa kupelekwa Muhimbili kwa
Matibabu zaidi.
“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI’
MAPINDUZI DAIMA
Issa Haji Usssi Gavu
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC
Idara ya Itikadi na Uenezi
ZANZIBAR
06/11/2012
Source: wavuti.com
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII