"SINA MPANGO WA KUGOMBEA URAISI"....JANUARY MAKAMBA

BongoNewz
January Makamba ndani ya studio za Magic FM akihojiwa na Fina Mango
Mbunge wa Bumbuli na Naibu waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia Mhe January Makamba amesema hana mpango wa kugombea Urais. Makamba aliyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha Makutano kinachoendeshwa na Fina Mango.

Alisema anaamini nafasi ya urais inahitaji mtu ambaye amejiandaa Kisaikolojia, Kisiasa na Kifikra na kumalizia kwa kusema kuwa Urais sio uamuzi wa mtu mmoja kwa sababu nchi haiendeshwi na mtu mmoja na inahitaji watu ambao wanashauriana, kuandaa dira ya pamoja na kupeleka ujumbe wa kuwaunganisha Watanzania.

Alipoulizwa Rais anayekuja anatakiwa aweje alisema anatakiwa awe ni mtu atakaewaunganisha Watanzania huku akisema mianya ya ukabila, udini na rushwa ambayo baba wa taifa Mwalimu Nyerere aliitaja imeanza kuonekana.

Pia Makamba alisema rais ajaye anatakiwa asiwe mtu mwenye hulka ya visasi na atakiwa awe na uwezo wa kuwaambia wananchi kuwa yeye sio masiha wa kuyafanya maisha yao yabadilike papo kwa hapo kwa kuwa nchi ni ya watu wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutumia nafasi yake kuleta mabadiliko.

Alipoulizwa katika wanasiasa wa upinzani ni yupi anamkubali, alimtaja Zitto Kabwe kwa sababu ana uwezo wa kusema na kusimamia kile anachokiamini, ujasiri wa kuomba ushauri kama kuna jambo ambalo halielewi na pia anapenda kusoma na kujifunza. Pia alitaja kuwa anamheshimu sana Profesa Ibrahim Lipumba.

Mheshimiwa Makamba alimalizia kwa kusema kuwa atagombea ubunge wa Bumbuli kwa kipindi cha pili na baada ya hapo atajikita katika shughuli za Shirika la Maendeleo ya Bumbuli (Bumbuli Development Corporation) alilolianzisha likiwa na lengo la kuleta washirika wa maendeleo ili kuwawezesha kiuchumi wananchi bila kutegemea miradi ya serikali.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs